Siku ya Ijumaa alasiri, mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo Gidi Ogidi alitangaza kwamba alikuwa akisafiri kuelekea eneo la Nyanza.

Mtangazaji huyo mahiri kupitia ukurasa wake wa Instagram alionyesha picha yake na watu wengine wawili akiwemo Mbunge wa Langata Phelix Odiwour walipokuwa wakijiandaa kupanda ndege kuelekea Kisumu.

Katika taarifa yake, Gidi alifichua kuwa lengo la safari yao lilikuwa kuhudhuria mazishi ya marehemu Willis Ayieko na mama wa rafikiye, ambao wote watazikwa Jumamosi.

“Wiki tatu zilizopita, tulikuwa Kakamega kusherehekea maisha ya Mama Esteri Mwenesi Ayiga, mama kwa rafiki yetu George Odanga. Marehemu Willis Ayieko alikuwa ajiunge nasi Jumamosi tarehe 20 kwa sherehe hiyo. Kwa bahati mbaya, aliuawa usiku wa kuamkia tukio hilo,” Gidi aliandika.

Aliongeza, “Siku chache baada ya sherehe, Mama Esteri alifariki alipokuwa akipokea matibabu Kisumu. Kwa hiyo kesho tuna maziko mawili. Mama Esteri huko Vihiga na Willis huko Alego wote siku moja.”

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Mtangazaji huyo wa Radio Jambo alizungumzia jinsi matukio hayo yalivyo huzuni na kuwatakia wafiwa faraja wanapowazika wapendwa wao.

“Inasikitisha sana. Familia za Mama Esteri na Willis zipate faraja. Tunaomba rehema za safari,” aliandika.

Takriban wiki mbili zilizopita, Gidi alithibitisha kuwa rafiki yake Willis Ayieko ambaye awali alikuwa ameripotiwa kutoweka aliuawa na watu wasiojulikana.

Marehemu alikuwa Meneja Mkuu wa Utumishi katika kampuni ya Wells Fargo.

“Inasikitisha sana. RIP rafiki yangu na jirani Willis Ayieko. Wauaji wako wasipate amani kamwe,” Gidi alisema kupitia mitandao ya kijamii.

Katika chapisho lingine, mtangazaji huyo mahiri wa redio alionyesha picha ya kumbukumbu marehemu Willis Ayieko akiwa na wanaume wengine wawili na kusema hiyo ndiyo ilikuwa picha yake ya mwisho.

Alithibitisha kuwa uchunguzi unaendelea kubaini kilichompata marehemu Ayieko na kuna matumaini ya kukamatwa kwa wahusika.

"Hii ni picha ya mwisho ambayo Willis (katikati) alipiga kabla ya kuondoka kwenda nyumbani kwa tukio la bahati mbaya. Uchunguzi unaendelea na tunatumai wahusika watakamatwa hivi karibuni. Tumepoteza rafiki mcheshi na mwenye huruma. Pumzika vizuri kaka ???,” Gidi alisema.