Wachezaji wa Chess kutoka nchi sita, yakiwemo Tanzania, Poland, Ujerumani, India, Nigeria na Msumbiji, wanatarajiwa kuchuana katika shindano la kupanda viwango la Shirikisho la Kimataifa des Echecs (FIDE).
Mashindano hayo yanayofanyika Desemba 14 na 15, ni mashindano ya mara ya nne ya kufanyika katika Chuo Kikuu cha Jordan mjini Morogoro mashariki mwa Tanzania.
Waandaaji wanajivunia uwepo wa timu hizo za kimataifa katika mashindano hayo, huku wakionyesha umuhimu wake katika kuinua hadhi ya Tanzania katika mchezo wa chess.
"Tunafuraha kuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka huu ambapo tayari tuna mataifa sita yamedhibitisha kushiriki," alisema Dkt Konrad Czernichowski, mmoja wa waandaaji na pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Jordan cha Morogoro.
Dkt Konrad aliongeza kuwa, “Pamoja na washiriki kutoka mataifa sita, ni fursa ya kipekee kuinua Tanzania kwenye jukwaa la dunia la mchezo wa chess. Viwango vya Chess sio nambari tu ni onyesho la ustadi, kujitolea, na huwa na hadhi ya kimataifa.”
Kabla ya kuanza kwa michuano hiyo, mchezaji wa mchezo wa chess kutoka Tanzania, Shedrack Mwakajila, ambaye hivi karibuni aliiwakilisha nchi yake kwenye Olympiad ya Chess mjini Budapest, alitembelea Klabu ya Jordan Chess na kucheza mchezo huo na wachezaji mbalimbali
Katika ziara yake, nyota huyo alikabiliana na wachezaji wengi mara moja dhidi yake na baadaye kucheza dhidi ya mchezaji mmoja mmoja. Wapinzani wawili tu ndio waliibuka washindi; mwanafunzi wa chuo hiko Inocent Agustino Herman na Dkt Konrad.
Dkt Konrad alimsifu Mwakajila kama mfano mzuri wa kuigwa na wachezaji chipukizi nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Dkt Konrad pamoja na washiriki wa kimataifa na fursa ya kupata viwango vya FIDE, mashindano ya Desemba yanatarajiwa kukuza wasifu wa chess wa Tanzania, kuwapa wachezaji wa ndani jukwaa la kimataifa na kuhamasisha vijana zaidi kujihusisha na mchezo huo.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!