Nahodha wa timu ya taifa ya ndondi ya Kenya Boniface Mugunde
Nahodha wa timu ya taifa ya ndondi ya Kenya, Boniface Mugunde ameonyesha furaha kubwa baada ya kunyakua taji la uzani wa light middle katika mashindano ya ndondi ya Bara Africa iliyokamilika nchini DRC, Kongo wiki iliyopita.

Mugunde aliorodhesha ushindi huo wa kihistoria baada ya kumzidi maarifa Nestor Nduwarugira wa Burundi katika kinyang'anyiro kikali katika ukumbi wa Stade des Martyrs mjini Kinshasa, DR Congo.

Kenya haikuwa imeshinda medali ya dhahabu tangu ushindi wa Nick Okoth katika uzani wa light fly nchini Congo Brazzaville mnamo 2017.

"Dhahabu hii ni ya Wakenya wote. Nina hakika huu ni mwanzo tu wa mafanikio makubwa zaidi katika mashindano yajayo," Mugunde alisema.

Aliwalimbikizia sifa wakufunzi wake kwa kumnoa vilivyo kwa ajili ya mashinano hayo. "Ninajivunia sana kupata dhahabu kwenye michuano ya Afrika, namshukuru Mungu na makocha wangu kwa mkakati ulionifanya niendelee katika kipindi chote cha pambano hilo na kuniwezesha kukwepa mtoano," Mugunde alisema.

"Njia za mafunzo makini, mwongozo wa uhamasishaji, na upangaji mkakati ulilipa vyema," Mugune alisema. Mugunde alielezea mafanikio yake kama ushahidi wa imani isiyoyumba. "Makocha wetu wamesisitiza mara kwa mara umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, nidhamu, na kazi ya pamoja, na falsafa hii imetoa faida," alibainisha.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kenya ilishinda medali mbili za fedha kupitia Elizabeth Andiego (uzani wa bantam) na Clinton Macharia (uzani wa juu).

Kenya pia ilijinyakulia medali za shaba kupitia kwa Amina Martha (uzani wa bantam), Abednego Kyalo (uzani wa fly), Vincent Ochieng (uzani wa light welter), Robert Okaka (uzani wa light heavy) na Shaffi Bakari (uzani wa feather).

Benjamin Musa, kocha mkuu, alimwagia mabondia wake sifa kemkem, akisema uchezaji wao bora unaonyesha kuwa nchi inarejea katika hadhi yake ya awali kwenye ulingo wa ndondi.

"Walionyesha uwezo na ukakamavu wao wakati wa shindano hilo. Ushindi wao umeinua ari yao na kudhihirisha umahiri wa ndondi wa Kenya," alisema.

Musa alielezea kufurahishwa kwake na kujituma na bidii ya mabondia hao, akiwemo Macharia ambaye aliibuka kidedea katika rangi za kitaifa.

"Mafanikio ya Macharia ni dhihirisho la talanta yake na azma yake. Ameonyesha uwezo wa kuwa maarufu katika ulingo," alisema.

Kwa kuzingatia historia tajiri ya ndondi nchini Kenya, Musa ana matumaini kuwa taifa hilo linaweza kurejesha nafasi yake ya kutawala mchezo huo.

"Ni wazi kuwa timu ya ndondi ya Kenya inaimarika, na taifa lina uwezo wa kurejesha nafasi yake ya ngumi zenye mwelekeo sahihi," alisema.