Mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 38 kutoka Milwaukee, Marekani anakabiliwa na mashtaka ya kumuua keshia wa duka la vyakula wakati wa mabishano kuhusu pizza Jumamosi, Oktoba 19.
Waendesha mashtaka walimshtaki Bw Charles Leggett kwa mauaji na kupatikana na bunduki kufuatia kisa hicho cha kushangaza.
Kisa hicho kinaripotiwa kutokea muda mfupi kabla ya saa sita mchana katika Action Food and Liquor karibu na King Drive na Keefe Avenue, mjini Milwaukee.
Kulingana na malalamiko ya jinai, mpiga simu kwa 911 alisema hakuona kilichotokea, lakini mtu aliingia na alikuwa akibishana na keshia.
Mpiga simu huyo alisema kuwa kisha alisikia mlio wa risasi moja na kumpata mwathirika kwenye sakafu nyuma ya kaunta.
Mwathiriwa alitambuliwa kama Jamil Owies mwenye umri wa miaka 26, ambaye alifariki katika eneo la tukio licha ya majaribio ya kuokoa maisha yake kutoka kwa watoa huduma ya kwanza.
Waendesha mashtaka walisema risasi iliyofyatuliwa ilipatikana kwenye sakafu karibu na mwili wake, na ganda moja la risasi la 9mm lilipatikana kwenye sanduku la peremende kwenye kaunta ya kulipia.
Kulingana na ripoti, mteja huyo aliyejawa na ghadhabu alimpiga risasi Bw Jamil hadi kumuua baada ya kupandwa na hasira kuhusu iwapo mpishi alivaa glavu alipokuwa akitengeneza pizza yake.
Leggett aliagiza pizza, akalipa kisha akachukua tikiti yake kuelekea nyuma ya duka, ambapo mtu mwingine alimwandalia pizza hiyo.
Lakini Leggett alirudi kwa keshia na kuanza kugombana kuhusu ikiwa mpishi alikuwa amevaa glavu kwani aliamini kuwa hakuwa nayo.
Leggett kisha akavuta bunduki, akafika juu ya kaunta na kuweka risasi kwenye kifua cha Jamil Owais kabla ya kukimbia.
Iwapo atapatikana na hatia, mshtakiwa anaweza kufungwa jela miaka 75.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!