Katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye kitengo cha Patanisho, jamaa kwa jina Asbel Kiptoo mwenye umri wa miaka 32 aliomba kupatanishwa na mke wake Junick Auma mwenye miaka 24.

Kiptoo alisema kwamba walikuwa wamekaa katika ndoa kwa kipindi cha miaka 2 lakini bado hawakuwa wamefanikiwa kupata mtoto.

Walikosana miezi mitano iliyopita baada ya Auma kuondoka nyumbani wiki mbili tu baada ya mumewe kuondoka akienda Nairobi kutafuta riziki.

Jamaa huyo alieleza kwamba mzozo ulianza katika ndoa yake baada ya kuondoka nyumbani na kumuacha mkewe ambaye baada ya wiki mbili pia aliondoka.

Kiptoo alisema kuwa awali walikuwa wanaishi Nairobi na wakarudi nyumbani Desemba iliyopita ambapo walikaa hadi Mei mume alipoamua kurudi Nairobi kutafuta riziki akimuacha mkewe nyuma.

Hata hivyo, wiki 2 baadae, mke naye aliondoka katika kile Kiptoo aliarifiwa na wakwe zake kwamba naye aliondoka kuenda Nairobi kivyake kujitafutia ajira sambamba na mumewe.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Mke wangu tulikosana, kwanza tulikuwa Nairobi kikazi ikafika Desemba tukaenda nyumba kuanzia Januari hadi Mei ikawa narudi nairobi. Nikamwambia akae nyumbani nirudi ndio aje baadae, sasa wakati nilikaa Nairobi wiki 2 nikapigiwa simu kutoka nyumbani wakaniambia ashatoka….” Kiptoo alieleza.

“Wakati nilimpigia simu hakuchukua nikafuatilia kwa wazazi wake hawakunijibu vizuri wakiniambia nilimuacha nyumbani na yeye alitoka kuenda kutafuta kazi, tangu hiyo siku tumekuwa tukisumbuana tu,” aliongeza.

Kwa upande wake, Junick Auma alipopigiwa simu, alisema kwamba “Ubaya Abel Kiptoo ni matusi ako nayo mingi, hadi anatusi mpaka mama mkwe na hiyo si vizuri. Hata tukiwa nyumbani nitoke nije kusalimia watu anaanza kuwaandikia matusi. Na hicho ndicho kitu kilinichosha,” alifichua.

Auma alimtaka Kiptoo kumpa muda kufikiria akisema kwamba bado ana hicho kidonda cha yeye kuwatukana wazazi wake.

“Bado nampenda lakini nataka tu anipe muda nifikirie. Hata ikiwa ni mpaka mwaka mmoja pia ni sawa. Unajua ni lazima niponye hicho kidonda, huyo mtu amenipeleka mbio sana, amesema vitu vingi lakini navumilia tu,” aliongeza.