Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi Gidi ametangaza kifo cha rafiki na jirani yake Willis Ayieko.

Katika taarifa yake Jumatano alasiri, Gidi alithibitisha kuwa rafiki yake ambaye awali aliripotiwa kutoweka aliuawa na watu wasiojulikana.

Marehemu alikuwa Meneja Mkuu wa Utumishi katika kampuni ya Wells Fargo. “Inasikitisha sana. RIP rafiki yangu na jirani Willis Ayieko.

Wauaji wako wasipate amani kamwe,” Gidi alisema kupitia mitandao ya kijamii. Katika chapisho lingine, mtangazaji huyo mahiri wa redio alionyesha picha ya kumbukumbu marehemu Willis Ayieko akiwa na wanaume wengine wawili na kusema hiyo ndiyo ilikuwa picha yake ya mwisho.

Alithibitisha kuwa uchunguzi unaendelea kubaini kilichompata marehemu Ayieko na kuna matumaini ya kukamatwa kwa wahusika.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

"Hii ni picha ya mwisho ambayo Willis (katikati) alipiga kabla ya kuondoka kwenda nyumbani kwa tukio la bahati mbaya. Uchunguzi unaendelea na tunatumai wahusika watakamatwa hivi karibuni. Tumepoteza rafiki mcheshi na mwenye huruma. Pumzika vizuri kaka ???,” Gidi alisema.

Marehemu Ayieko aliondoka jijini Nairobi mwendo wa saa saba mchana mnamo Ijumaa, Oktoba 18, lakini hakufika nyumbani, jambo lililozua wasiwasi kuhusu aliko. Alitarajiwa kuhudhuria hafla Kakamega Jumamosi, Oktoba 19, lakini hakufika.

Familia yake ilikua na wasiwasi simu zake zilipozima, na hakuna mtu aliyeweza kumpata. Siku kadhaa baadaye, bado hakukuwa na dalilia za yeye kupatikana. Wikendi iliyopita, mtangazaji Gidi alikuwa amewataka Wakenya kumwombea Willis ambaye alikuwa ameripotiwa kutoweka. "Maombi kwa ajili ya rafiki yetu Willis Ayieko," alisema.

Polisi wameanzisha uchunguzi baada ya mwili wa marehemu Willis kupatikana.