
FKF inashirikiana na shirika la habari la Radio Africa Group na runinga ya TV47 kuandaa mdahalo huu mkubwa zaidi utakaowakutanisha wote ambao wamewasilisha barua zao kwa shirikisho wakilenga kiti cha urais.
Mdahalo huo utafanyika katika ukumbi wa chuo kikuu cha Katoliki na utapeperushwa moja kwa moja kupitia kituo chako pendwa cha Radio Jambo Ijumaa hii ya Oktoba 25 kuanzia saa kumi na mbili thenashara.
Wanajopo waliothibitishwa kwa mjadala huu muhimu ni pamoja na: Barry Otieno, Chris Amimo, Sammy Owino, Sam Nyamweya, Sam Ochola, Hussein Mohammed, Doris Petra, Cleopas Shimanyula, na Tom Alila – wote wakiwa na nia moja ya kuwa rais wa shirikisho la FKF.
Mjadala huu unatarajiwa kuwafikia Wakenya milioni 20 na unawakilisha wakati muhimu katika kuunda mustakabali wa soka katika nchi ya Kenya. Katika barua rasmi kuthibitisha kuandaliwa kwa mdahalo huo mkubwa nchini, FKF ilisema imewaalika washikadau wote wa spoti kushuhudia kivumbi wagombea wakinadi sera zao kwa umma moja kwa moja kupitia Radio Jambo.
“Tunawaalika wanahabari, wadau, na umma kusikiliza Redio Jambo na TV47 kwa kile kinachoahidi kuwa mazungumzo ya kuleta mabadiliko,” barua hiyo ilisema kwa sehemu.
“Majadiliano hayo yanalenga kutoa maarifa ya uwazi kuhusu jinsi kila mgombea anavyopanga kuimarisha na kusaidia soka katika ngazi zote,” FKF iliongeza.
Shirikisho hilo liliweka wazi kwamba linatambua mpira wa miguu ni msingi wa utambulisho wetu wa kitaifa, hivyo mjadala utashughulikia mada muhimu, zikiwemo: Ukuzaji wa vipaji vya vijana, Ufadhili wa mpira wa miguu wa ngazi ya chini, Uadilifu katika utawala wa soka, bila kusahau Ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi katika kuendeleza mchezo.
Usikose kufuatilia mdahalo huu mkubwa wa kihistoria kusikiliza jinsi mgombea unayempigia upato atakuwa anadadavua sera zake mbele ya jopo la washikadau shakiki wa soka.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!