Raia wa Uingereza ameiambia BBC kuwa yeye na wenzake kadhaa raia wa Uturuki walitekwa nyara na watu waliojifunika nyuso zao siku ya Ijumaa jijini Nairobi Kenya.
Waturuki wanne kwa sasa hawajulikani waliko.
Necdet Seyitoğlu, ambaye aliishi nchini Uingereza kwa miaka 18 kabla ya kuhamia Kenya miaka miwili iliyopita, alisema aliachiwa baada ya saa nane alipowaonyesha wanaodaiwa kumteka nyara nakala ya pasipoti yake ya Uingereza.
Katika taarifa, Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilisema "wanatoa usaidizi wa kibalozi kwa Muingereza na familia yake kufuatia tukio lililotokea nchini Kenya".
Kulingana na ripoti hiyo, "watu wanane waliokuwa na silaha walitoka kwenye magari hayo mawili, na kuwatoa watu wawili waliokuwa ndani" na kuondoka nao, alisema msemaji wa polisi wa Kenya Resila Onyango.
"Baadaye, Yusuf Kar mmoja, raia wa Uingereza mwenye asili ya Uturuki" aliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi kilicho karibu na kuwataja watu waliotekwa nyara kuwa ni Hüseyin Yeşilsu na Necdet Seyitoğlu.
Mamlaka ya Uturuki bado haijatoa maoni yoyote kuhusu tukio hilo.
Tukio hilo linachunguzwa na Mamlaka ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI.
Tawi la Nairobi la Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kuhudumia Wakimbizi pia limethibitisha kwamba “UNHCR imepokea ripoti na itatoa taarifa zaidi pindi tutakapozipata.”
Watu waliopotea walisemekana kuwa chini ya ulinzi wa Umoja wa Mataifa jijini Nairobi.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!