Siku
ya Ijumaa jioni, Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Kalerwa Salasya alitangaza
kupata kazi nzuri ya ubalozi ambayo itaongeza mapato yake ya kila mwezi.
Katika
chapisho kwenye mitandao wa kijamii, mwanasiasa huyo kijana alifichua kwamba
alikuwa ametia saini mkataba wa ubalozi na kampuni ya mali isiyohamishika yenye
makao yake makuu jijini Dubai.
Salasya
alichapisha video inayomuonyesha akikutana na mwakilishi wa Capital Partners na
akafichua kuwa atakuwa akipokea Sh400,000 kila mwezi kutoka kwa kampuni hiyo
baada ya kutia saini mkataba wa ubalozi.
"Wakati kukiwa na shughuli nyingi za kumbandua naibu rais nilikuwa bize kusaini mikataba ya nafasi ya balozi wa chapa ya kampuni kubwa ya kimataifa ya mali isiyohamishika ya dubai! 400k kwa mwezi ni ushindi wangu!!! Tujengane,” Salasya alisema.
Huku akiongea kwenye video iliyochapishwa na Salasya, mwakilishi wa kampuni hiyo alifichua kuwa wananuia kutambulisha mradi wao nchini Kenya.
Aliendelea kumshukuru mwanasiasa huyo kijana na kumsifu kwa athari alizoleta kwenye hafla yao.
"Asante kwa watu kama wewe, umefanikisha sana," mwakilishi huyo alisema.
Salasya ni miongoni mwa wabunge waliokuwa wakipinga vikali kutimuliwa kwa aliyekuwa naibu wa rais , Rigathi Gachagua.
Wakati hoja ya kumtimua ilipowasilishwa bungeni na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, mbunge huyo wa awamu ya kwanza aliipinga huku wenzake wengi wakipiga kura kuunga mkono.
Baada ya hoja hiyo kupitishwa bungeni wiki jana, mwanasiasa huyo mcheshi alichukua muda kuwasihi Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na mwenzake wa Busia Okiya Omtatah kupiga kura dhidi ya kuondolewa kwa Gachagua madarakani.
Salasya alimwonya Sifuna kwamba kwa kuunga mkono kuondolewa kwa DP, anaweka taaluma yake ya kisiasa hatarini.
“Nataka kukukumbusha ndugu yangu, Edwin Sifuna, una chaguzi za kuchagua ‘Ndiyo’ ili kufurahisha chama cha ODM au ‘Hapana’ ili kuokoa azma yako ya muda mrefu ya kisiasa. Usipoteze maeneo bunge haya saba ya Nairobi, unayahitaji na Wakenya kwa jumla ambao hawaoni sababu ya kushtakiwa kwa Gachagua,” Salasya alisema.
Katika ombi lake kwa Omtatah, Salasya alibainisha kuwa Seneta wa Busia anaaminiwa na kupendwa na Wakenya wengi na kwamba walikuwa wakimtegemea.
Maseneta mnamo Alhamisi jioni hata hivyo waliendelea kuunga mkono hoja ya kuondolewa madarakani kwa Gachagua, na kumfanya kuwa DP wa kwanza wa Kenya kutimuliwa.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!