Waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki sasa ni naibu rais mteule.

Hii ni baada ya wabunge 236 kupiga kura kuidhinisha uteuzi uliyofanywa na rais William Ruto akimpendekeza Kindiki kuwa naibu Rais siku ya Ijumaa.

Hatua hii sasa inamaanisha kuwa rais Ruto anaweza wakati wowote kumteua rasmi Kindiki kuwa naibu rais kuchukuwa nafasi ya Rigathi Gachagua. Baada ya uteuzi rasmi naibu rais mteule ataapishwa katika hafla ambayo itashuhudiwa na jaji mkuu.

Kindiki ndiye Waziri wa sasa wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa. Jina lake liliwasilishwa kwa Bunge la Kitaifa mnamo Ijumaa. Spika Moses Wetang'ula alitangaza uteuzi huo katika Kikao maalum kilichoandaliwa Ijumaa.

“Nimepokea ujumbe kutoka kwa rais kuhusu uteuzi wa Profesa Kithure Kindiki kujaza nafasi iliyoachwa wazi katika afisi ya Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya,” Wetang’ula alisema.

Wetangula aliambia bunge kuwa hoja ya uteuzi wa naibu rais kulingana na kanuni za bunge ilihitaji kupigiwa kura moja kwa moja.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

"Kanuni za Bunge katika mchakato huu ni kwamba Bunge litaenda moja kwa moja kupiga kura bila kushirikisha umma. Kwa ajili hiyo, kwa mujibu wa Kifungu cha 149(1) cha Katiba, Bunge linapiga kura baada ya kupokea uteuzi, na hitaji la kushirikishwa kwa umma halitumiki. "Kwa kiwango ambacho Kifungu cha 149(1) cha katiba kinazingatia Bunge kupiga kura baada ya kupokea uteuzi, hitaji la ushiriki wa umma halitumiki katika hali hii," Wetang'ula aliongeza.

Aliyekuwa naibu Rigathi Gachagua alibanduliwa mamlakani na bunge na kisha uamuzi huo kuthibitishwa na seneti. Gachagua atayari amewasilisha kesi kadhaa kupinga kung’atuliwa kwake.