Rais William Ruto amemteua Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kama Naibu Rais mpya kufuatia kutimuliwa kwa Rigathi Gachagua Alhamisi usiku.

Jina la Kindiki liliwasilishwa Bungeni Ijumaa asubuhi ambapo wabunge wanatarajiwa kulipigia kura kuidhinisha.

Spika Moses Wetang'ula alitangaza uteuzi huo katika Kikao maalum kilichoandaliwa Ijumaa asubuhi.

“Nimepokea ujumbe kutoka kwa rais kuhusu uteuzi wa Profesa Kithure Kindiki kujaza nafasi katika afisi ya Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya,” Wetang’ula alitangaza.

Katiba inasema pindi rais akishawasilisha uteuzi kwenye Bunge, wabunge watapiga kura ya kulikataa au kuliidhinisha jina hilo. Pia hakuna sharti la kura ya thuluthi mbili.

Kisha mteule ataapishwa kuwa ofisini baada ya kuidhinishwa.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kindiki amekuwa akihudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani kwa takriban miaka miwili.

Hapo awali alihudumu kama Seneta wa Kaunti ya Tharaka Nithi kwa mihula miwili (miaka 10).

Katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022, Kindiki alikuwa miongoni mwa waliopendekezwa kuwa mgombea mwenza wa Ruto lakini hatimaye akaamua kumchagua Gachagua.

Baadaye rais alieleza kwamba alimchagua Gachagua kwa sababu ya umri wake na alifikiri wangeelewana zaidi.