Mchungaji wa Kenya mwenye utata mwingi Paul MacKenzie, kwa mara nyingine tena amesisitiza onyo ambalo alitoa baada ya kukamatwa mwaka jana.

MacKenzie ambaye kwa sasa anazuiliwa katika gereza la Shimo la Tewa alifikishwa kortini siku ya Jumatano wakati aliposikika akijigamba kuhusu onyo lake la awali.

“Si unaona tu kinawaramba, si unaona tu Kenya inarambwa, ama namna gani? Kenya inarambwa hii,” MacKenzie alisikika akisema huku akitabasamu.

Kiongozi huyo wa kanisa la Good News International Ministries anaaminika kuwa alikuwa akirejelea hali ya mambo ya sasa katika taifa la Kenya.

Mackenzie alitoa onyo la ‘Kitawaramba’ kwa mara ya kwanza wakati akiwa kwenye gari la polisi muda mfupi baada ya kukamatwa Aprili 15.

Alisikika kwenye video akiwaonya polisi na watu waliokuwa wamekusanyika karibu na gari la polisi kutoliangalia suala hilo kwa sababu litakuja kuwasumbua.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Mnachopigana nacho hamkijui na kitawaramba, kitawaramba nawaambia,” alisema.

Tamko hilo lilionekana kuwa tishio, na haraka likawa maarufu. Wakenya waliitumia kuwaonya wengine kwamba huenda jambo baya likawapata kwa matendo yao.

Neno hilo lilionekana kulingana na kupanda kwa gharama ya maisha.

Neno hilo pia lilitumiwa katika mitazamo mingine marafiki wanapoambiana kwamba kitu kitaenda vibaya au wanafanya uamuzi mbaya ambao unaweza kuwaandama baadaye.

Neno hilo la mzaha lililotumiwa na Mchungaji Paul Mackenzie mnamo Aprili 25, 2023, lilifika kwenye orodha ya Neno la Mwaka la Associated Press (AP) mnamo 2023.

Kasisi huyo mwenye utata alishtakiwa kwa kuongoza ibada ya siku ya maangamizi ya njaa ambayo ilisababisha vifo vya zaidi ya watu 400.