Mwanaharakati wa haki za kibinadamu, Eric Omondi amefichua kwamba mipango yake ya kuandaa sherehe ya Mashujaa Dei, sambamba na ile itakayoandaliwa na serikali ingali katika hatua za lala salama.


Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Eric Omondi alisema kwamba siku ya Mashujaa ambayo itakuwa Jumatatu wiki kesho, yeye na wafuasi wake watakuwa katika uwanja wa Uhuru eneobunge la Lang’ata kaunti ya Nairobi.


Mwanaharakati huyo alisema kwamba dhima itakuwa kuwasherehekea vijana wa Gen Z waliofariki katika maandamano ya kupinga serikali.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans


Omondi aliwataja vijana hao waliofariki, wengi wao mikononi mwa maafisa wa kupambana na ghasia, kama mashujaa wa kizazi kipya ambao wanastahili kutambuliwa na kusherehekewa vilivyo.


“Tunatoa wito kwa Wakenya kutoka Kona zote za Taifa hili kuungana nasi tunapoadhimisha MASHUJAA WETU WALIOFARIKI, katika bustani ya Uhuru Jumapili hii tarehe 20. Kila Kizazi kina Mashujaa wake na hawa ni Wetu. Kubeba Bendera na Mshumaa. Programu Inaanza saa 9:00. USIKOSE,” Omondi alitangaza.


Haya yanajiri wakati ambapo serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Kwale ikiendelea maandalizi ya kufanyika kwa sherehe za Mashujaa.


Mashujaa Dei ya mwaka huu itafanyika katika kaunti ya Kwale, ikiwa ni mara ya kwanza sherehe hizo kufanyika katika kaunti hiyo tangu ugatuzi, mwaka 2013.


Mashujaa Dei husherehekewa kila mwaka Oktoba 20, kusherehekea mashujaa waliopigania uhuru wa Kenya.